​LITA YATAKIWA KUWA CHANZO CHA ELIMU BORA YA MIFUGO

Imewekwa: 05, May 2022

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda ameitaka Wakala ya Elimu ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kuwa chanzo cha elimu bora ya mifugo ndani na nje ya nchi.

Bw. Nzunda amesema hayo jijini Dodoma (28.03.2022) wakati akifungua rasmi kikao cha tisa cha Baraza Kuu la Wafanyakazi la LITA na kubainisha kuwa ni wakati sasa wakala hiyo kuwa chanzo cha kuwashauri wafugaji na kutoa maarifa kwa wadau wa sekta ya mifugo ili sekta hiyo iweze kuimarika na kuwa ya kisasa zaidi.

Ameongeza kuwa wakufunzi wa LITA wanatakiwa pia kuwa chanzo cha kuandaa majarida mbalimbali vikiwemo vitabu vya ufugaji na kuwa chanzo cha kubuni na kupatikana kwa maarifa mapya yanayotokana na tafiti zinazofanywa na wakufunzi hao.

Aidha, katibu mkuu huyo amefafanua kuwa wajibu wa LITA ni kuwa karibu na umma kwa kutoa huduma bora ikiwemo ya wanafunzi wanaohitimu kuwa bora na wanaoheshimika, kutambulika, wenye maarifa, wanajiamini na kuandaliwa vizuri kwenda kusaidia sekta binafsi.

Awali Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi la LITA Dkt. Pius Mwambene, akizungumza kabla ya ufunguzi rasmi wa kikao hicho amesema wakala hiyo imeendelea kuimarisha mahusiano na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha inaboresha miundombinu ya kufundishia.

Dkt. Mwambene ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa LITA amefafanua kuwa kwa sasa wakala hiyo inakaribia kukamilisha makubaliano ya ujenzi wa kampasi ya LITA Mkoani Songwe ikiwa ni jitahada za kuongeza wigo wa elimu ya mifugo katika maeneo mbalimbali nchini.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha wafugaji wanapata mwongozo wa ufugaji bora LITA imeanisha utaratibu wa kuwashikiza wanafunzi wa hatua ya nne kwa wafugaji katika maeneo yao wakati wa likizo ili kuanza kujenga uzoefu ujasiri wa kuwahudumia wafugaji mapema.

Pia, amebainisha kuhusu vikao vya Baraza Kuu la Wafanyakazi LITA, kuwa vinalenga kuishauri wakala kutekeleza majukumu yake kama ilivyoelekezwa kwenye sheria, kupokea na kujadili makadirio ya mapato kwenye matumizi ya wakala na kujadili mipango ya utekelezaji wake kwa ajili ya ustawi wa wakala na wafanyakazi wake.

Kufuatia malengo hayo amewataka wajumbe wa baraza kushiriki kikamilifu na kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya wakala.

Akitoa neno la shukran baada ya kufunguliwa rasmi kwa kikao cha tisa cha Baraza Kuu la Wafanyakazi LITA, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa amesema wataendelea kusimamia maadili na weledi kwa wafanyakazi wa LITA na kuongeza ushirikishwaji ili kuwa na matokeo makubwa yenye maslahi mapana yatakayoleta tija.

Dkt. Mwilawa amefafanua kuwa nguvu zaidi zitaelekezwa kwenye maeneo ambayo yatagusa jamii na kwamba maelekezo yote yatafanyiwa kazi kwa kuweka vigezo na kupima vizuri ili kufikia malengo.

Amesema kuwa kila mfanyakazi aliyepo LITA atahakikisha anapata stahiki zake ili aweze kutekeleza majukumu yake kama anavyotegemewa katika kutoa mafunzo ya elimu bora ya mifugo kwa wanafunzi.

Nao baadhi ya wajumbe wa baraza katika kikao hicho, wametoa maependekezo kadhaa ya kuboresha utendaji kazi pamoja na mazingira ya wafanyakazi ili waweze kufanya kazi kwa morali na kufikia malengo ya LITA.

Wamesema kikao hicho ni muhimu katika kukumbushana utekelezaji wa mambo mbalimbali yakiwemo ya kiutawala kwa kuwashirikisha wafanyakazi na kutatua kero na kuwapatia taarifa sahihi kwa wakati ili kuondoa manung’uniko kazini.