Imewekwa: 22, January 2026
Wakala ya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) imeandaa na kuendesha warsha ya kuanza mchakato wa uandaaji wa Mtaala wa Teknolojia za Uzalishaji Kuku kwa kufanya Upembuzi wa mahitaji ya stadi zinazohitajika kufundishwa kwa Wataalam katika mnyororo wa thamani wa kuku. Lengo la Warsha hii ni kuchambua na kupata maoni ya wadau kuhusu stadi na ujuzi (situational analysis) katika tasnia ya kuku.
Warsha hiyo imefanyika Januari 20, 2026 katika Ukumbi wa Wakala ya Maabara ya Vetenari Tanzania (TVLA), na imewakutanisha Wadau muhimu wakiwemo Wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi; Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Uholanzi; Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Wawakilishi kutoka Vyama vya Wafugaji Kuku nchini; Makampuni yaliyopo katika mnyororo wa thamani wa kuku (Silverland, Alvine, Interchick, Falcon); Wataalam kutoka MSM; Wafugaji; Wakufunzi kutoka LITA na Vyuo Binafsi.
Akizungumza katika warsha hiyo, Naibu Mkuu wa Chuo LITA, Bw. Balija Luyombya amewasilisha malengo na matarajio ya Warsha kuwa ni kupata maoni na kupitisha stadi zinazohitajika na wadau zitakazojumuishwa katika Mtaala. Naye Dkt. Edward Mneda wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), aliwasilisha mwaongozo na hatua za kuzingatia katika uandaaji wa mitaala.
Aidha, katika maelezo ya awali Bw. Sebastian Shilangalila Mwakilishi kutoka Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani alieleza kuwa warsha hii ni hatua muhimu kwa wadau kutoa maoni kwa kuzingatia mahitaji halisi ya sekta ya mifugo, hususan katika kuandaa wataalam wenye stadi, ujuzi na weledi wa kushauri, kujiajiri, kuajiri katika mnyororo wa thamani wa kuku. Hivyo, aliwaasa wadau kushiriki kikamilifu na kutoa maoni yatakayotumika katika kuandaa mtaala.