Imewekwa: 08, May 2026
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena, amewataka Watumishi wa Taasisi ya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uweledi, ubunifu, uchapakazi na uhadilifu mkubwa ili kuweza kuleta matokeo chanya katika Taasisi yao na Sekta ya Mifugo kiujumla.
Akizungumza leo Mei 8, 2026 Jijini Dodoma katika Mkutano wa Kumi na Tatu (13) wa Baraza Kuu la Wafanyakazi LITA, Bi. Meena amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaitegemea LITA katika kuleta chachu ya mabadiliko ambayo itasaidia kuboresha Sekta ya Mifugo na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa.
"Ili kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi ni muhimu kuwa na watumishi ambao wanajituma na kutekeleza wajibu wao kama ambavyo inatakiwa kwa uadilifu na kwa wakati" amesema Bi. Meena
Aidha, Bi. Meena ameitaka LITA kuwa wabunifu zaidi na kuimarisha ushirikiano na Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi, katika kuboresha Taasisi yao ili kuweza kuimarisha Sekta ya Mifugo, na ametoa wito kwa LITA kuwapatia wakufunzi wao Mafunzo ya kisasa ambayo yataendana na Mfumo wa sasa wa Kiteknolojia ili kuweza kuendana na kasi ya sasa ya ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia.
Vilevile, Bi. Meena ameipongeza menejimenti ya LITA kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufunza katika baadhi ya Kampasi zake, pamoja na kutekeleza Miradi ya ujenzi na ukarabati ambao unatekelezwa katika baadhi ya kampasi ili kuendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa LITA, Dkt. Pius Lazaro Mwambene amesema LITA imeendelea kuboresha Mitaala ambayo imeanza tayari kutumika katika mwaka huu mpya wa masomo, Mitaala ambayo imekuja na teknolojia nyingi mpya.
Pia, Dkt. Mwambene amesema kutokana na Mitaala hiyo mipya ya teknolojia, LITA imeanza mchakato wa kuwapeleka wakufunzi wao kwenye Mafunzo ili kuendana na kasi hiyo ya teknolojia mpya, na hii inatokana na ushirikiano wa LITA na Taasisi zingine zikiwemo za kutoka nchi ya Hungary ambayo inawapeleka wakufunzi mbalimbali nchi za nje kupata Mafunzo hayo